BLAGNON KUIKOSA MWADUI FC NA STAND UNITED

Mshambuliaji wa kikosi timu ya Simba aliyesajiliwa msimu huu akitokea Ivory Coast  Frederic Blagnon anatarajiwa kukosa mechi mbili za timu hiyo kutokana na jeraha la kuchanika juu ya jicho alilopata kwenye mechi dhidi Toto Africans Jumamosi.

Mshambuliaji huyo amepewa siku saba za kuuguza jeraha lake hivyo kulazimika kuwa nje ya kikosi kilichosafiri jana kwenda mkoani Shindanga ambapo Simba itacheza mechi mbili dhidi ya wenyeji wake Mwadui FC na Stand United.

Simba wanatarajiwa kuanza kusaka pointi sita muhim mkoani Shinyanga siku ya Jumamosi kwa kukwaana na Mwadui FC kwenye uwanja wa Kamabarage Nyerere. Na siku ya Jumatano watakuwa kwenye uwanja huohuo kuwavaa Stand United.

Akielezea kuhusu maendeleo ya mchezaji huyo, daktari wa Simba, Yasin Gembe amesema kuwa walimshona nyuzi nne ila kwa sasa anaendelea vizuri na wamempa siku saba za mapumziko ili jeraha lake lipone.

Blagnon aligongana na beki wa Toto Yusuf Mlipili kwenye mchezo ambao Simba wakiwa wenyeji waliibuka na ushindi wa 3-0 dhidi Toto, mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es salaam.