KOCHA MZAMBIA AIKANA YANGA

George Lwandamina aliyetua nchini juzi akitokea kwao Zambia, akitajwa kuwa amekuja kujiunga na Yanga kuchukua mikoba ya Hans Van Pluijm ya kuifundisha timu hiyo ya Jangwani, ameukana uvumi huo na kusema kuwa amekuja nchini kwa shughuli zake binafsi za kibiashara na wala si kujiunga na Yanga.

Hata hivyo habari za uhakika kutoka kwenye kilabu hiyo zinasema kuwa Mzambia huyo tayari ameshamalizana na Yanga na anatarajiwa kuanza kazi wakati wowote.

Taarifa za uongozi wa Yanga kuingia makubaliano na kocha huyo zilianza kuzagaa kama wiki tatu zilizopita hasa baada ya mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya mahasimu wake Simba SC.

Tayari aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mholanzi Hans Van Pluijm, mapema jana aliwasilisha barua ya kuomba kujiuzulu kwa uongozi. Barua hiyo imepokelewa na amekubaliwa kujiuzulu. Na inawezekana wakati wowote Mzambia huyo akatangazwa kuinoa timu hiyo inayopambana kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.