SIMBA YAENDELEA KUCHANJA MBUGA

Na Victor Mahudi

Vinara waligi kuu Simba SC ya Dar es salaam jana waliendeleza rekodi yao ya ushindi katika mbio za ligi kuu ya Vodakom Tanzania Bara kwa kuifunga Mbao FC ya Mwanza bao moja kwa bila.

Bao la Simba lilifungwa dakika 86 na Kiungo Mzamir Yassin aliyesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Mzamir alifunga goli hilo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Fredrick Blagnon ambaye pia amesajiliwa msimu huu akitokea Ivory Coast.

Simba walianza kulishambulia lango la wapinzani wao tangia kipindi cha kwanza, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Mbao pamoja na uhodari wa kipa Emmanuel Mseja aliyeokoa michomo kadhaa ya washambuliaji wa Simba ndiyo ilichelewesha ushindi kwa wekundu hao wa Msimbazi.

Dakika ya 60 ya mchezo Blagnon aliifungia Simba bao lakini likakataliwa na refa Hance Mabena kutoka Tanga kwa madai kuwa aliunawa mpira kabla ya kufunga.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 26 hivyo kuimarisha uongozi wake kwenye msimamo wa ligi kuu ya Vodacom.