YANGA YAELEKEZA NGUVU ZAKE KAGERA SUGAR

Kocha wa kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara Yanga Africans ya Dar es salaam, Hans van der Pluijm amesema kuwa, sasa hivi wanaelekeza nguvu zao kwenye mechi ijayo dhidi Kagera Sugar ya Bukoba Kagera.

Yanga ambayo Juma tano ya ya wiki hii ilikwaana na Toto Africans katika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na kushinda 2-0, keshoJuma Mosi itakuwa ugenini kwa mara nyingine kumenyana na Kagera Sugar, mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba.

Pluijm amesema kuwa matokeo waliyopata kwenye mechi ya juzi yanawapa nguvu na hali kushinda mechi zinazofata.

Akizungumzia kuhusu kikosi chake, Pluijm amesema kuwa ataendelea kukifanyia mabadiliko ya mara kwa mara kwa kubadilisha badilisha wachezaji kulingana na mechi husika ili kumpa kila mchezaji wa kikosi hicho nafasi ya kucheza na kupumzika.

Amesema kuwa kuna wachezaji kama Oscar Joshua, Hassan Kessy na Haruna Niyonzima ambao aliwapumzisha mechi kadhaa za nyuma, lakini mechi ya Toto Africans aliwapanga na wakacheza vizuri kutokana na kuwa walipata muda wa kupumzika.

Yanga itahitaji kushinda mechi ijayo ili iweze kujiwekea mazingira mazuri ya kutetea ubingwa msimu huu.